Tuesday 9 December 2014

Tubuni basi mkarejee…



“Tubuni basi mkarejee…dhambi zenu zifutwe zipate kuja nyakati za kuburudishwa” Matendo ya Mitume 3:19

Mtu mmoja aliwahi kusema “Haujawahi kutokea ugonjwa hatari duniani kama dhambi.” Idadi ya watu waliopoteza maisha kwa ajili ya dhambi ni kubwa kuliko idadi ya watu waliokufa kwa ajili ya Malaria na UKIMWI.


Katika Warumi 6:23 inasema mshahara wa Dhambi ni mauti. Neno mshahara hapa laweza kutafsiriwa kuwa “malipo ya ya dhambi ni  kifo.” Neno kifo pia laweza kutafsiriwa kuwa mtu kukosa furaha, maendeleo, kukosa amani nk. Hivyo ni kusema malipo ya Dhambi ni ugumu wa maisha, magonjwa kama vile (HIV/AIDS), kukosa maendeleo, kukosa amani, ndoa kuvunjika, kuongezeka kwa ajali, mauaji, ugaidi nk.

Tangu anguko la mwanadamu pale Edeni maisha yamekuwa ya kukatisha tamaa, majuto nk. Katika dunia nzima kila mtu anatamani kupata maisha mazuri ya amani, maendeleo, furaha, afya nk. Dawa ya kusaidia kuondoa dhambi ambayo ndiyo asili ya mabaya yote inatafutwa. Mtume Paulo anakutana na mazingira kama hayo na anatoa majibu kwa kusema “TUBUNI.”


Nini maana ya neno hilo? Neno “Tubu” linamaanisha “Geuka” “badili mwelekeo” kama ulikuwa unaenda kushoto geuka uende kulia. Kwa minajili hiyo neno hili linatuita kuyaacha yote yanayotufanya tumkosee Mungu na kuyatenda yale yanayompendeza yeye.

Petro anatufundisha katika 1Petro 3:10-11 juu ya toba inayoleta matunda. Jiulize wewe unatafuta wapi maisha mazuri? Anasema maisha mazuri na siku njema huja kwa:

i. Kuzuia ulimi usinene mabaya

ii. Midomo yako isinene uwongo

iii. Acha mabaya tenda mema

iv. Tafuta amani, uifuate sana

 Leo kweli wengi tumegeukia kutafuta maisha na siku njema kwenye rushwa, waganga, ufisadi, umalaya, ugaidi, wizi, uchawi, utapeli nk. Neno la Mungu linasema tubu yaani geuka-usitende hayo tena.

Tunapotubu Mungu anamtuma Yesu kwa njia ya Roho wake Mtakatifu kutuburudisha. Tena kwa njia hiyo tunapata baraka. Historia ya maisha yetu inabadilika. Badala ya kilio huja kicheko, badala ya laana huja baraka.

Ndugu mpendwa wako mamilioni ya watu ambao wamegundua siri hii kwa kufanya hivyo wamebadili historia ya Maisha yao. Sasa wanayo furaha na Tumaini la maisha ya hapa duniani na hata baadaye huko mbinguni. Ni vyema ukaisikia sauti ya Mungu inayokuita wewe kutubu (geuka) sema sala hii Bwana atakusikia na kukufanya kiumbe kipya.

“Mungu baba yetu wa mbinguni, nasogea mbele zako nikiyajutia maovu yangu yote. Nakuomba unirehemu na kunisafisha na uovu wangu wote unipe nguvu ya Roho wako mtakatafu ili aniwezeshe kuwa na mwenendo mpya wa kukupendeza wewe. Tangu leo niwe mwana wako. Kwa Kristo Bwana wetu”. Amen.

Sasa umekuwa kiumbe Kipya. Ikiwa unahitaji msaada zaidi waweza kwenda kwa kiongozi wa kanisa lililoko karibu nawe au kupiga simu kwa namba zifuatazo.

0754855769

0752010436

0763997146

0769165722

0765750523

0 comments:

Post a Comment